Back to top

Aliyetoroka magereza na kufanya ujambazi auawa.

20 November 2020
Share

Izack Kawogo mkazi wa Njombe mjini ameuawa na Jeshi la Polisi usiku wa kuamkia Novemba 20 akituhumiwa kujihusisha vitendo vya uporaji na ujambazi kwa kutumia silaha.


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe Hamisi Issa amethibitisha na kubainisha kuwa marehemu kabla ya kushambuliwa na polisi waliokuwa doria alimjeruhi kaka yake anaefahamika kwa jina la Andrea Kawogo (61) kwa kumpiga risasi mbili begani kwa kutumia silaha aina ya SMG Uzgun.

Kamanda pia amesema marehemu alikuwa na matukio ya unyang'anyi kipindi cha nyuma jambo ambalo lilipelekea kufungwa jela miaka 30 na kisha kuhamishiwa gereza la Iringa ambako alimjeruhi askari magereza kwa panga na kisha kutoroka na silaha hiyo ikiwa na risasi kumi.


Aidha Kamanda huyo amesema wakati uchunguzi unafanyika ili kumnasa mtuhumiwa ndugu walikuwa wazito kutoa ushirikiano licha ya kujua maovu yake jambo ambalo limesababisha kuchelewa kumdhibiti.