Back to top

Askari JWTZ,Polisi mbaroni kwa rushwa mkoani Kagera.

22 October 2019
Share

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) katika mkoa wa Kagera inamshikilia askari mmoja wa jeshi la wananchi wa Tanzania na mwingine wa jeshi la polisi ambao ni miongoni mwa watu wanne wanaokabiliwa na tuhuma ya kujihusisha na makosa ya kuomba rushwa kutoka kwa wananchi ambao ni wakazi wa wilaya ya Biharamulo.

Hayo yameelezwa na mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Kagera, John Joseph aliyemtaja askari wa jeshi la wananchi anayeshikiliwa kuwa ni Koplo Nyambita Magoma mmoja wa wakufunzi wa ofisi ya mshauri wa mgambo wilayani Biharamulo aliyeomba rushwa ya shilingi milioni 3 kwa mtu ambaye mifugo yake ilikutwa kwenye hifadhi ya msitu wa Biharamulo na Koplo Nassor Mirambi askari polisi aliyeshirikiana na Asaph Manya kuomba rushwa ya shilingi 700,000 kutoka mchoma mkaa aliyekutwa na magunia 50 na amemtaja mwingine anayeshikiliwa kuwa Audastus Norbert afisa afya aliyeomba rushwa ya 200,000 ili asifunge bucha ya mfanyabiashara wa nyama. 
 
Mkuu huyo wa TAKUKURU ameendelea kuwahimiza wananchi katika mkoa huo waendelee kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo juu ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na amewaomba wanapotoa taarifa za vitendo vya rushwa wawe wanajitokeza mahakamani kutoa ushahidi ili watu hao watiwe hatiani.