Back to top

"DIRA YA TAIFA 2050 ITAMBUE MAHITAJI YA VIJANA"DK.MPANGO

08 June 2024
Share

Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Mpango amesema Dira 2050 ni muhimu itambue mahitaji ya vijana na kubeba  matamanio yao, ili kuifanya iwe ya vijana zaidi na kwa ajili ya vijana kwa kuwa ndio kundi kubwa la watu nchini.
 
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa kuhusu Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lililofanyika katika Ukumbi wa Nkurumah – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 imebainisha wazi kuwa 77.5% ya watanzania ni vijana, hivyo ni muhimu Dira na mikakati yake ya utekelezaji ibainishe fursa na changamoto za muundo na mwenendo huo wa idadi ya watu katika Taifa.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa makongamano ya kupokea maoni ya kuwezesha utekelezaji wa Dira kujielekeza katika kutatua tatizo kubwa la utegemezi uliopo hivi sasa wa 87.4%, ikimaanisha  ni sehemu ndogo tu ya nguvukazi ya Watanzania ndio inayobeba mzigo mkubwa wa mahitaji ya msingi ya kundi kubwa la wategemezi na hivyo kudidimiza kiwango cha Taifa cha kuweka akiba kwa ajili ya kujenga mitaji ya uwekezaji.

Pia amesema ni muhimu kuangazia namna bora ya kutumia nguvu kazi kubwa ya vijana kuharakisha maendeleo pamoja na kuweka nguvu kwenye maendeleo ya elimu ya kujenga ujuzi, stadi za kazi, teknolojia na upanuzi wa shughuli zinazovutia vijana, ikiwemo zinazotumia TEHAMA, Sanaa na Burudani, uwezeshaji wa shughuli zinazochipukia na kilimo janja.
 
Aidha Makamu wa Rais amesema ni muhimu Dira 2050 ibainishe uwezo na fursa kubwa za nchi kwa kuzingatia mahitaji ya ndani na nje ya nchi. 

Amesema eneo la kutazamwa kwa karibu ni rasilimali kubwa za madini zilizopo nchini na uvunaji wa madini hususan ya kimkakati unapaswa upangwe kwa umakini mkubwa ili kuweza kunufaisha zaidi Taifa, kwa kuweka viwanda vya uchenjuaji wa madini hayo na kutengeneza bidhaa  kama betri za magari ya umeme, bidhaa na vifaa mbalimbali vya kielektroniki, sumaku, mitambo ya kufua umeme kutokana na upepo pamoja na vifaa na vipuli vinavyotumika katika vifaa vya kisasa kama ndege na roketi. 

Amesema ni muhimu kuyafanya madini hayo kutumika kwa ajili ya kujenga uwezo wa ndani katika kutengeneza bidhaa mbalimbali badala ya kuyasafirisha yote kwenda nje.