Back to top

DKT.SAMIA ADHAMIRIA KUFANYA MAPINDUZI YA SEKTA YA UVUVI

17 November 2023
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, amepania kuifanya sekta ya Uvuvi kuwa moja ya sekta vinara katika kukuza uchumi wa nchi.

Mhe.Mnyeti amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi boti 2 za Uvuvi zenye thamani ya shilingi milioni 158.5 kwa wavuvi wa mikoa ya Rukwa na Katavi iliyofanyika kwenye Mwalo wa Nankanga wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mhe. Mnyeti amesema kuwa kitendo hicho ni ishara ya nia ya dhati ya Rais Samia ya kuonesha kwa vitendo maono yake ya kuibadilisha sekta hiyo na kuifanya itekeleze shughuli zake kwa tija jambo ambalo halikuwahi kufanyika huko nyuma.

Mhe.Mnyeti amewataka wavuvi hao kutumia boti hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa huku pia akiwapa rai ya kujiepusha na uvuvi haramu na kuingia kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kuvuliwa kisheria.

Akizungumza kwa Niaba ya Wavuvi wa mkoa wa Katavi, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Mhe.Onesmo Buswelu mbali na kumshukuru Mhe. Rais Dkt.Samia kwa mkopo huo usio na riba wa boti za uvuvi ameahidi kusimamia matumizi ya vyombo hivyo ili viweze kuwa na tija kwa wavuvi wa mkoa huo.

Naye Bw.Onesmo Mahundi ambaye ni Mvuvi wa Kijiji cha Nankanga mkoani Rukwa, ameishukuru Serikali kwa mkopo huo ambapo amesema kuwa yeye na wenzake wataitumia boti hiyo kubadili mfumo wao wote wa shughuli za uvuvi.

Zoezi la ugawaji boti nyingine mbili za uvuvi linatarajiwa kuendelea kesho katika mwalo wa Kasanga uliopo wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.