Back to top

FAO kushirikiana na Tanzania kuinua sekta ya kilimo nchini.

12 January 2019
Share

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeahidi kuendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania katika kuinua sekta ya kilimo nchini.

Mwakilishi wa shirika hilo hapa nchini Fred Kafeero ametoa ahadi hiyo alipokutana na Naibu Waziri wa Kilimo,Mhe.Innocent Bashungwa katika ofisi za FAO jijini Dar es Salaam.

Amesema shirika hilo limekuwa lishirikiana na serikali ya Tanzania katika kutunga sera na kuandaa mikakati yenye lengo la kuhakikisha Tanzania inasonga mbele katika kilimo.
 
Amesema katika miaka ya karibuni limefanya kazi kwa ukaribu na Shirika la Takwimu Tanzania kwa kulijengea uwezo wa ndani unaoisaidia pia serikali katika ufuatiliaji wa bei ya mazao nchini.
 
Kwa upande wake Mhe.Bashungwa amemueleza muwakilishi huyo mpango wa serikali wa kuorodhesha wakulima wote nchini ili kuweza kupanga vizuri kuhakikisha kila mkulima anapata huduma muhimu zitakazomsaidia toka hatua za uandaaji shamba mpaka masoko na kuliomba shirika hilo kuipa serikali ushirikiano ombi ambalo mwakilishi huyo wa FAO ameahidi kulifanyia kazi.