Back to top

KENYA: NDEGE ZAGONGANA ANGANI, WAWILI WAFARIKI

05 March 2024
Share

Watu wawili  waliokuwa ndani ya ndege aina ya Cessna mali ya Ninety-Nines Flying School ambao ni Rubani Mwanafunzi na Mkufunzi,  wamefariki dunia baada ya kugongana na ndege  nyingine angani jijini Nairobi.

Ndege hiyo ilianguka katika Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi,  na kuwaua wawili hao papo hapo.

Ndege ya pili, waliyogongana nayo  ni Dash 8, mali ya  Safarilink Aviation Limited, ambayo imethibitisha kuwa ilikuwa ikielekea Diani,  ikiwa na abiria 39 na wafanyakazi 5 hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa katika ndege hiyo.

 Wafanyakazi wa  ndege hiyo waliamua kurejea mara moja kwenye Uwanja wa Ndege wa Nairobi-Wilson kwa ukaguzi na tathmini zaidi na walitua salama.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (KCAA) tangu wakati huo imeanza uchunguzi kubaini hali iliyosababisha ajali hiyo ya angani.