Back to top

Kituo kikubwa cha ukuzaji wa viumbe maji kujengwa Chato.

09 July 2020
Share

CHATO MKOANI GEITA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah amesema serikali inatarajia kujenga Kituo kikubwa cha ukuzaji wa viumbe maji Wilayani Chato, Mkoani Geita, huku akisema kuwa kituo hicho kitakuwa kinatoa zaidi ya tani 10 za samaki kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa kukabidhi eneo la ujenzi wa kituo hicho kwa kampuni ya ukandarasi ya serikali, Corporation Sol Julai 8, 2020 katika kijiji cha Rubambangwe, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, Dkt.Tamatamah amesema kuwa mradi huo mpaka kukamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.8 na tayari Wizara imeshalipa fidia ya shilingi milioni 42 kwa wakazi wa eneo hilo ambalo linaukubwa wa ekari 28.

Ameongeza kuwa mradi huo ambao unategemewa ujenzi wake kuchukua miezi 3 na kukamilika Oktoba, 2020 utakuwa jengo la vitotoleshi vya samaki ambalo litakuwa na uwezo wa kutoa vifaranga zaidi ya milioni mbili kwa mwaka.

Naye Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Viumbe Maji, Dkt.Nazaeli Madala amesema kuwa kituo hicho kitakuwa ni ufumbuzi wa changamoto ya uhaba wa samaki ulioanza kujitokeza kwenye vyanzo vya asili.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka mradi huo katika Wilaya hiyo na aliahidi kufuatilia kwa ukaribu hatua zote za ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika.