Back to top

Maafisa ugani watakiwa kuongeza usimamizi wa mashamba ya Korosho

16 September 2020
Share

Kituo cha utafiti wa kilimo TARI Naliendele kimetoa rai kwa maafisa ugani kuongeza usimamizi wa mashamba ya wakulima ili kuondokana na magonjwa na wadudu wanaoshambulia zao la Korosho, huku kukiwa na viwatilifu vyenye uwezo wa kutibu magonjwa hayo.

Kauli hiyo imetolewa na mtafiti wa magonjwa na wadudu kutoka kituo cha utafiti wa kilimo TARI Naliendele wakati akitoa elimu ya wadudu na magonjwa yanayoshambulia zao la Korosho katika wilaya ya Tandaimba.

Amesema magonjwa pamoja na wadudu waharibifu wa mkorosho wanasababisha zaidi ya asilimia hamsini ya mavuno yote kupotea shambani na hivyo mkulima kupata hasara.

Hata hivyo amesema magonjwa sio tatizo wala wadudu sio tatizo na kusisitiza tatizo ni kukosekana kwa usimamizi na ufuatiliaji  unaotakiwa kufanywa na mabwana shamba pamoja na mabibi shamba .

Amesema madawa ya kupambana na wadudu pamoja na magonjwa ya mkorosho yaliyothibitishwa na mamlaka husika yapo hivyo hakuna sababu ya mashamba ya wakulima kuendelea kuzongwa na magonjwa na hivyo kuwa sehemu ya kushusha uzalishaji wa zao hilo.

Kwa upande wao maafisa ugani wamesema wamekuwa wakifanya ufuatiliaji ila changamoto kubwa ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakichangia uwepo wa magonjwa ambayo hawana utaalamu nayo.