Mahakimu watakiwa kuzingatia haki za binadamu mashauri ya ukatili

Msajili mkuu wa mahakama Tanzania Katarina Revocat amewataka mahakimu wa mahakama zote nchini  pamoja na taasisi zote zinazohusika na utoaji wa haki kuhakikisha wanatoa haki stahiki katika mashauri ya uvunjifu wa haki za binadamu hasa ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto kwa kuzingatia sheria na mikataba ya kimataifa bila kujali mila na desturi ambazo nyingine zimekuwa kandamizi na kuyaathiri makundi hayo.

Akizungumza mjini Kigoma wakati wa mafunzo maalumu yanayoendeshwa na chama cha majaji na mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kuwashirikisha majaji, mahakimu, mawakili pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na utoaji haki nchini ,huku akisema ipo haja ya wadau kushirikiana kikamilifu ili kutokomeza vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto. 
 
Mkuu wa dawati la jinsia la polisi mkoa wa kigoma mrakibu wa polisi Amina Kahando amesema kumekuwa na jitihada kubwa kuhakikisha vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto vinatokomezwa kwa kuwashirikisha wadau na jamii, baada ya mkoa wa kigoma kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo.