
Waziri Mkuu Mh.Kassim Majaliwa amewataka wazazi wahakikishe vijana wao wanakwenda kusoma kwenye shule za sekondari kwani bila elimu hawawezi kufika mbali.
“Wazazi wenzangu hakikisheni vijana wenu wanaenda shule. Hatuwezi kufika mbali kama vijana wetu hawaendi shule. Tunajenga shule kila mahali, tunataka maeneo yote yawe na shule,” Mh.Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambiranje, Ruangwa mkoani Lindi.
Akielezea utekelezaji kwenye sekta ya maji, Waziri Mkuu alisema vijiji vyote 90 vya wilaya vilichimbiwa maji kupitia taasisi ya GAIN lakini kwa sasa hayatoshi, lakini alisema serikali imetoa bilioni 49 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka Nyangao ambao utavinufaisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 29 vya wilaya ya Nachingwea.
Kuhusu umeme, alisema kwamba laini zimeshaenda kwenye kila kijiji na kwamba Serikali hivi sasa inashughulika kuweka umeme kwenye ngazi ya vitongoji. “Leo hii hakuna kijiji kisichokuwa na umeme.”
Kuhusu barabara, alisema kuna changamoto ya barabara kufika katika kijiji cha Mtondo ambayo tayari iko kwenye mpango wa ujenzi. “Kuna barabara ya kutoka Mandawa Chini hadi hapa, Nanjalu hadi hapa, Nambiranje hadi hapa na kutoka Namiyenje hadi hapa.