Back to top

Majaliwa:Tumedhamiria kuboresha miundombinu ya Bandari.

20 July 2021
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya bandari ili kuvutia idadi kubwa ya watumiaji zikiwemo nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Ameyasema hayo alipokutana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, Mkurugenzi wa Bandari, TASAC, TBS, TMDA, Kamishna wa Forodha pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya usafirishaji.

Amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika uboreshwaji wa huduma mbalimbali bandarini zikiwemo za upakuaji wa mizigo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mizigo yote inayopitia bandarini inapakuliwa katika kipindi cha muda mfupi.

Amesema bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zimefanyiwa maboresho makubwa, hivyo amewasisitiza wadau wa sekta binafsi waendelee kuleta meli za kutosha.

Aidha Waziri Mkuu amesema mbali na maboresho yaliyofanyika katika bandari hizo, pia bandari za Kabwe, Kasanga nazo zimeboreshwa pamoja na ujenzi wa bandari ya Karema ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria katika nchi za Congo, Zambia na Burundi.