Back to top

Mashamba ya Mirungi yateketezwa Kilimanjaro.

11 December 2021
Share

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro wamefanya oparesheni maalum ya kuharibu mashamba ya mirungi zaidi ya hekari 10 katika Kitongoji cha Kindi Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza Kiongozi wa Oparesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Bw. Gerald Kusaya amesema Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti wamejipanga katika kuhakikisha wanapambana kwa kila namna katika kudhibiti biashara hiyo lengo likiwa ni kumaliza kabisa athari zitokanazo na matumizi ya dawa hizo.


Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ACP. Simon Marwa Maigwa amesema katika kipindi cha kuanzia Mwezi Januari mpaka Septemba mwaka 2020, jumla ya kesi 540 za dawa za kulevya ziliripotiwa Mkoani humo na watuhumiwa 467.

Pia Kamanda Maigwa amesema katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2021 jumla ya kesi 678 ziliripotiwa huku watuhumiwa wakiwa 561 ambapo kesi hizo zipo katika hatua mbalimbali mahakamani ikiwemo kwenye Mahakama ya uhujumu uchumi.

Aidha amewaomba wananchi kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya dawa hizo ambazo zinaathiri nguvu kazi ya Taifa.