Back to top

MFUGAJI WA MFANO TANGA AWEZESHWA MALISHO YA KISASA 

08 April 2024
Share

#VIDEO:Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa upande wa sekta ya Mifugo, imemuwezesha mfugaji wa mfano jijini Tanga Bi Mariam Shekue kilo 250 za malisho ya mifugo, aina ya Nepia iliyoboresha maarufu kama Juncao.

Akielezea hatua za upandaji wa aina hiyo ya malisho, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizarani hapo, Dkt. Asimwe Rwiguza amesema kuwa awali ya yote mfugaji anapaswa kuandaa shamba lake na kulisafisha kwa kutumia jembe la mkono, wanyama kazi au trekta ili kuhakikisha linakuwa safi.

"Hatua ya pili ni kulainisha udongo kwa kutumia trekta ili mfugaji atakapopanda mbegu zake ziweze kuota kwa urahisi kisha atandaa vipimo kwa kutumia kamba ambapo kama anaandaa shamba kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za malisho anashauriwa kupanda kwa upana na urefu wa sentimeta 100 kati ya shina na shina lakini kama anapanda kwa ajili ya kuzalisha malisho ya mifugo anashauriwa kupanda kwa upana wa sentimeta 60 kati ya shina moja na jingine na mstari mmona na mwingine" Amefafanua Dkt. Asimwe.

Aidha Dkt. Asimwe amewaondoa hofu ya gharama wafugaji wanaotaka kulima malisho hayo kwani vifaa vingi vinavyotumika vinaweza kupatikana kwenye mazingira yanayowazunguka.

"Kwa mfano wakati wa kuandaa vipimo tunatumia vitu vinavyopatikana shambani kwa sababu tunatumia mti mbichi ambao umenyooka vizuri na utaukata kwa vipimo vya sentimenta 100 na mwingine kwa kipimo cha sentimenta 60 hivyo hata kama una shamba kubwa kiasi gani bado unaweza kupima kwa urahisi kabisa na ukapanda malisho yako" ameongeza Dkt. Asimwe.

Akizungumza mara baada ya kupandiwa malisho hayo shambani kwake, Bi. Mariam Shekue ameishukuru Wizara kwa kutambua juhudi zake kwenye ufugaji ambapo ameahidi kutumia shamba lake kama darasa kwa wafugaji wengine.

Naye Afisa Mifugo wa Mkoa wa Tanga Bw. Issa Hatibu amewataka wafugaji wengine mkoani kwake kuendelea kuzalisha malisho ya mifugo yao ili kuepukana na migogoro ya matumizi ya ardhi na kufuga kisasa.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara yake ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo imekuwa ikiwahamasisha wafugaji wake kulima malisho ya kutosha na kuyahifadhi kwa ajili ya mifugo yao ili kuwa na uhakika wa upatikanaji chakula hicho wakati wa kiangazi.