Back to top

Mgombea Urais wa CHADEMA aahidi kuivunja NEC akiingia madarakani.

25 September 2020
Share

Harakati za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA Tundu Lissu kutafuta uongozi wa nchi, zimeendelea katika majimbo ya Misungwi, Kwimba, Sumve, Magu na Nyamagana mkoani Mwanza, huku  akiahidi kuwa iwapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao, ataivunja Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na kuitisha upya uchaguzi wa serikali za mitaa.


Mgombea urais huyo kwa tiketi ya CHADEMA ameyasema hayo katika mkutano wake wa kampeni mjini Misungwi, baada ya msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo kuwaengua wagombea udiwani wote wa kata 27 za jimbo hilo pamoja na mgombea ubunge wa chama hicho Shija shimbi .

Akiwa Hungumalwa wilayani Kwimba, mgombea urais huyo wa Jamhuri ya Muungano Mh. Tundu Lissu amesema akichaguliwa kuongoza nchi atakomesha mfumo wa Stakabadhi Ghalani aliodai unawakandamiza wakulima .

Akihutubia wakazi wa jiji la Mwanza katika uwanja wa Kleruu Mabatini, Mgombea Urais huyo, ametangaza neema kwa watumishi wa vyombo vya dola, wakiwemo wanajeshi, askari polisi na kada zingine za elimu na afya, ambao amedai kwa miaka mitano iliyopita hawajawahi kupewa nyongeza ya mishahara.