Back to top

MKONGE KUWA ZAO LA KIMKAKATI KWAONGEZA HAMASA

20 November 2023
Share

Mwaka 1964, historia inaonesha zao la Mkonge kama zao la kilimo limeshawahi kuiingizia nchi ya Tanzania Asilimia 65 ya Fedha za kigeni. Haijawahi kutokea kwa zao lingine la kilimo kufanya hivyo hapa nchini. Kifupi zao la mkonge lilikuwa linaingiza pesa nyingi zaidi za kigeni kuliko bidhaa nyingine zilizokuwa zinauzwa nje ya nchi kwa wakati huo.

Ni katika kipindi hicho ambacho Tanzania ilikuwa ikizalisha Tani Laki Mbili na Elfu Thelathini ya zao hilo huku ikielezwa kuwa kwa uzalishaji huo uliifanya Tanzania kuwa nchi kinara kwa uzalishaji wa zao hilo Duniani.

Kufuatia historia hiyo,  inaonesha wazi kuwa bado nchi ya Tanzania inayo nafasi kubwa  ya kujipanga vyema, kuongeza uwekezaji ili kuimarisha uzalishaji wa zao hilo na nchi ikarudi tena katika nafasi ya kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha kwa wingi zao hilo ulimwenguni.

Akizungumza katika Kongamano la Uwekezaji, Biashara na Utalii pamoja na Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji lililofanyika Mkoani Tanga mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Bw. Saddy Kambona alisema kuwa katika jitihada za kuinua uzalishaji wa zao hilo ambao kwa muda mrefu ulikuwa umeshuka, kuanzia mwaka 2019 Serikali ilitangaza zao hilo kuwa la kimkakati huku ikiweka msukumo mkubwa katika kuwahamasisha wakulima wadogo kuingia katika kilimo cha zao hilo.

Bw.Kambona aliongeza kwa kusema kuwa tangu wakati huo mpaka sasa muitikio wa wananchi kulima zao hilo ni mzuri sana na eneo la wakulima wadogo limeongezeka ambapo mpaka sasa hekta elfu 20 zimeshalimwa na wakulima wadogo na mkonge huo upo katika hatua mbalimbali za uzalishaji.

Aliendelea kufafanua kuwa hatua hiyo ya wakulima wadogo kulima hekta hizo Elfu 20 kunapelekea sasa kutengeneza fursa kubwa ya uhitaji wa uwekezaji wa mashine mbalimbali za uchakataji wa zao hilo la mkonge.

"Hii ni fursa kubwa kwa wananchi na wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika mitambo ya kuchakata mkonge ili kujiingizia kipato kwani kwa sasa hivi wastani wa gharama za kuchakata Tani moja ya zao la mkonge ni kiasi cha shilingi Laki 8 hadi milioni 1,  hivyo unaweza kuona  ni fursa kubwa kiasi gani", alisema

Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa  rai kwa wananchi na wawekezaji mbalimbali kuendelea kujitokeza kuikimbilia  fursa hiyo huku akisema kuwa Bodi ya Mkonge ipo tayari kuwasaidia kuwapa takwimu za mkonge unaofaa kuvunwa na kuwaelekeza maeneo ambayo kwa sasa yanafaa kuwekeza  mashine hizo.

Mpaka sasa, fursa ya nchi kuendelea kuingiza dola kupitia zao hilo ni kubwa. Serikali ya Rais, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan imesimama kidete kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaimarika na kuongezeka, lililo muhimu ni wananchi kutumia fursa hiyo kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa zao hilo ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja.