Back to top

MNH YAZINDUA JARIDA LA TAFITI ZA AFYA

12 December 2025
Share

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imezindua rasmi jarida lenye tafiti mbalimbali zinazofanywa hospitalini hapo, na kuelezwa kuwa kila mwaka MNH hupokea maombi ya tafiti kati ya 400 hadi 500 zinazohusu maeneo tofauti ya huduma za afya, tiba na ustawi wa jamii. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jarida hilo uliofanyika hospitalini hapo, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo, amesema Muhimbili ina jukumu muhimu katika kuboresha ubora wa huduma za afya nchini na kuimarisha sera za kitaifa kupitia tafiti hizo. 

“Hatuwezi kuboresha huduma kama hatuna tafiti, zinatufanya tujue wapi tuweke kipaumbele. Jarida hili ni  hatua muhimu ya kuonesha kazi kubwa inayofanywa na wataalam wetu katika kukuza ushahidi wa kitaalam" amesema Dkt Kimambo. 

Aidha ameongeza kuwa tafiti hizo husaidia kubaini changamoto za kiafya zinazoikabili jamii na kuweka misingi ya kuboresha huduma kwa kutumia ushahidi. Pia zinachangia kujenga uwezo wa kitaaluma kwa wafanyakazi wa afya nchini kupitia ushiriki wao katika kufanya na kuchambua tafiti hizo.

Kwa upande wake Afisa Muuguzi MNH, Bw. Anord Nyanana, ambaye amefanya utafiti kuhusu majeraha ya moto yanayohusiana na kupikia na matumizi salama ya gesi ya kimiminika ya petroli jijini Dar es Salaam, amesema utafiti una mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko katika sekta ya afya nchini.

“Baada ya kuona ongezeko la wagonjwa waliolazwa wakiwa na majeraha ya moto yaliyosababishwa na gesi ya kupikia, niliamua kufanya utafiti ambao unaweza kusaidia kuboresha ubora wa huduma, kujenga uwezo wa kitaaluma, kuimarisha sera za kitaifa na kuanzisha huduma za kisasa zinazowafikia watu wengi,” amesema Bw. Anold

Jarida hilo limejumuisha jumla ya tafiti 130 zinazohusu masuala mbalimbali ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza, afya ya mama na mtoto, saratani, ubunifu wa kiteknolojia na maboresho ya mifumo ya utoaji huduma hospitalini.