Back to top

Mtu mmoja auawa kwa kushambuliwa na Tembo wilayani Tunduru.

22 May 2018
Share

Mkazi wa kijiji cha Malumba wilayani Tunduru mkoani Ruvuma Zuberi Mahochi ameuawa kwa kushambuliwa na Tembo wakati akijaribu kumfukuza Tembo katika shamba lake katika kijiji cha Misyaje jirani na hifadhi ya wanyamapori ya Chingoli huku vijiji vitano vikizingirwa na Tembo na kusababisha wananchi waishi kwa hofu wilayani humo.

ITV imefika katika kijiji cha Misyaje na kuzungumza na ndugu  wa marehemu ambapo mama mdogo wa marehemu Fatma Ally pamoja na kuzungumzia masikitiko ya kumpoteza ndugu yake anaiomba serikali kuwalinda dhidi ya tembo kwa kuwa wanaishi kwa hofu.

Vijiji vitano vinavyosumbuliwa na Tembo ni kijiji cha Masyaje kulikotokea kifo ,Mkowela,Hulia Makande  na kijiji cha Rahaleo na hapa mwenyekiti wa kijiji cha  Mkowela Bw. Suleiman Somanga  anasema wananchi mbali na kupoteza mazao yao lakini wanaishi kwa hofu ya kuuawa na Tembo.

Mkuu wa  wilaya ya Tunduru Bw. Juma Homera aliyetembelea eneo la tukio  na kushiriki  maziko ya  marehemu Mahochi anasema kuwa serikali kwa kushirikiana na idara ya wanyamapori,mamlaka inayoshughulikia wanyamapori(TAWA),kikosi dhidi ya ujangiri(KDU)Pams foundation wanawarejesha Tembo kwenye  hifadhi.