Back to top

NDAKI AFICHUA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA KWENYE SEKTA ZA MIFUGO

05 August 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki amesema Wizara yake imetambulisha teknolojia itakayowawezesha wadau wa tasnia ya maziwa kupima ubora wa maziwa kwa urahisi na haraka kabla ya kuidhinishiwa kibali cha kuuza au kuyatumia.
  
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki ametumia jukwaa la ufunguzi wa maonesho ya Nanenane kanda ya Pwani Mashariki uliofanyika, mkoani Morogoro kuweka wazi mabadiliko ya teknolojia ambayo yamefanywa na Wizara yake kupitia sekta za Mifugo na Uvuvi.

Mhe.Ndaki ameyasema hayo wakati akielezea ushiriki wa Wizara yake kwenye Maonesho ya Nanenane kwa upande wa kanda hiyo ambapo amebainisha kuwa baada ya kubaini changamoto kubwa inayowakabili wadau wa sekta ya Mifugo hasa kwenye ukataji wa vibali na maombi ya leseni za biashara, Wizara yake iliamua kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama “MIMIS” ambao unamuwezesha mdau huyo kupata huduma zote kupitia simu yake ya mkononi bila kufika ofisini au kusubiri kwa muda mrefu kama ilivyokuwa awali.

"Tunataka kutoka kwenye mifumo ya awali ya kusajili kwa kutumia makaratasi na ndio maana kupitia Nanenane ya mwaka huu, tunasisitiza wadau wetu wa mifugo wafike kwenye mabanda yetu ili waweze kujifunza mfumo huu unaohusisha pia usajili wa wadau mbalimbali waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo"Amesema Mhe. Ndaki.

Akigusia maendeleo ya teknolojia yaliyofanyika kupitia sekta ya Uvuvi, Mhe.Ndaki amesema kuwa hivi sasa Wizara yake imeanza matumizi ya teknolojia ya kubaini vifaranga wa samaki wenye jinsia moja "Unisex" ambayo itamsaidia mfugaji wa samaki kujua aina ya samaki anaotaka kufuga jambo ambalo lilikuwa ni changamoto hapo awali.

"Lakini pia tumeleta teknolojia nyingine ya ukaushaji wa dagaa kwa njia ya jua hizi zote zipo kwenye mabanda yetu hivyo mtakapopita mtapata fursa nzuri ya kujifunza namna zinavyofanya kazi na niwaombe sana Watanzania wote tuanze kuondoka kwenye mifumo ile ya zamani na kuanza kutumia hizi teknolojia mpya kwa sababu zitaturahisishia kazi zetu za Ufugaji na Uvuvi" Amesisitiza Mhe.Ndaki.

Katika hatua nyingine Mhe.Ndaki amebainisha kuwa kwa mwaka huu wa Fedha Wizara yake inatarajia kuanzisha vituo atamizi 10 vitakavyowajumuisha vijana wa kike na kiume 240 wanaojihusisha na masuala ya Ufugaji jambo ambalo anaamini litapunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa upande wa kundi hilo.

"Vituo hivi vitakuwa na ruzuku hivyo niwaombe sana wananchi na hasa vijana wa kike na wa kiume kujitokeza kwa wingi pindi mtakapopewa taarifa na wataalam wetu ili mjiunge kwa wingi kwenye vituo atamizi hivi ambavyo mbali na kuwawezesha kupata ajira pia vitawapa fursa ya kupata mtaji wa Elimu, ujuzi na Weledi kwenye masuala ya ufugaji"Amesema Mhe. Ndaki.

Maonesho hayo ya Nanenane kanda ya Pwani Mashariki yamefunguliwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda na yanaendelea kwenye Viwanja vya Nanenane mkoani Morogoro ambapo yanatarajiwa kufikia kilele chake Agosti 8, 2022.