Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dakta Hussein Ali Mwinyi amesisitiza dhamira ya serikali anayoingoza ya kufungua uchumi na kuongeza makusanyo ya kodi, ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
.
Amesisitiza hayo alipolihutubia taifa kutoka viwanja vya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
.
Amesema katika kufungua uchumi, serikali inakusudia kuwavutia wawekezaji, kupanua uwekezaji na kuimarisha uvuvi wa kisasa kwa kutumia kikamilifu rasilimali kuu ya bahari ambayo Zanzibar imejaliwa kuwa nayo.
.
Aidha, ameelezea azma ya serikali ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia kupanua huduma za elimu na afya na kuongeza kiwango cha malipo kwa wazee.
.
Rais Dakta Mwinyi amerudia wito wake kwa wananchi wa kutimiza wajibu wao na kutoa ushirikiano kwa serikali ya umoja wa kitaifa aliyoiunda kwa mujibu wa katiba, ili kuiwezesha kuwaletea maendeleo na ustawi wa wananchi.