RC aagizwa kuunda Timu ya kupitia uuzaji kahawa.

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali, Charles Mbuge aunde timu maalumu itakayofanya mapitio ya mfumo mzima wa uuzaji wa zao la kahawa wilayani Ngara.

 Ametoa agizo hilo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa uuzaji wa zao hilo unaosimamiwa na Chama cha Msingi cha Wakulima wa Kahawa Ngara ambacho kimekuwa kikiwakata wakulima makato mengi na kuwapunguzia tija.

“Makato mengi mnayowakata wakulima hayana msingi kwa mkulima, mfano wa makato hayo ambayo yanakatwa katika kila kilo moja ya kahawa ya mkulima ni pamoja na riba ya mkopo unaokopwa na chama hicho (36%), usafirishaji (34%), gharama za ukoboaji (shilingi 112), gharama ya usafirishaji nje (1%).”  

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha Ngara Coffee Abdallah Seif ameiomba Serikali iwape kibali kitakachowaruhusu kununua kahawa kwa wakulima kwa bei nzuri tofauti na ilivyo sasa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwalinda wenye viwanda nchini na haitavumilia kuona wawekezaji wakinyanyaswa.