Back to top

SERIKALI YAGAWA PIKIPIKI 300 KWA MAAFISA UGANI NCHINI.

17 January 2022
Share

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amekabidhi Pikipiki Mia Tatu (300) kwa Wakuu wa Mikoa 25 ili zikatumiwe na Maafisa Ugani wa sekta ya mifugo waliopo katika Halmashauri kwa lengo la kuwarahisishia kazi ya kuwahudumia wafugaji nchini.

Mhe. Dkt.Mpango alikabidhi pikipiki hizo muda mfupi baada ya kufungua Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma. 

Wakati akikabidhi pikipiki hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Athony Mtaka kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wengine, Dkt. Mpango  alisema kuwa sekta ya mifugo ni moja kati ya sekta za kipaumbele kwa serikali, na ugawaji wa pikipiki hizo kwa maafisa hao ni katika jitihada za serikali kuboresha sekta hiyo ili iweze kuwa na tija kubwa kwa Taifa.

"Serikali inatambua changamoto za sekta hii, napenda kuwahakikishia serikali inaendelea kuzitatua na ndio maana leo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kununuliwa kwa pikipiki hizi, na tutaendelea kuboresha huduma za ugani ikiwemo kuendelea kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji wetu,” amesema Dkt.Mpango

Ametumia nafasi hiyo kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Manispaa kutenga fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za maafisa ugani katika maeneo yao huku akiwataka maafisa ugani hao kuhakikisha wanazitumia vyema pikipiki hizo ili kuwasaidia wafugaji kufanya ufugaji wenye tija.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema pamoja na kazi kubwa inayofanyika ya kuboresha sekta hiyo ya mifugo, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya maafisa ugani na hivyo alimuomba Makamu wa Rais kuona uwezekano wa serikali kutoa kibali cha ajira kwa ajili ya maafisa ugani.

"Mhe.Makamu wa Rais pamoja na uwepo wa teknolojia ya ugani kiganjani, haiondoi uhitaji wa maafisa ugani, uhitaji ni mkubwa, tunaomba serikali iwaajiri maafisa hawa ili waje kusaidia wafugaji wetu huko waliko"amesema Mhe.Ndaki

Kuhusu pikipiki hizo, Mhe.Ndaki amesema serikali imetumia Shilingi Milioni 864 kununua pikipiki hizo na zitasambazwa kwa mikoa 25 na  Halmashauri 140 zinatarajiwa kufaidika na pikipiki hizo.