
Kamati ya taifa inayokusanya maoni juu ya matumizi ya sera mpya ya nyumba na makazi imeitaka serikali kuanzisha vyeo vipya vya maafisa ardhi na mipango miji wa vijiji na kata ili kuondoa migogoro mingi inayosababishwa na baadhi ya maafisa ardhi wa wilaya ambao walio wengi hawaendi vijijini.
Mtaalam wa ardhi wa kamati hiyo Profesa Alphonce Kyesi ametoa rai hiyo kwenye mkutano wa wadau wa ardhi wa kanda ya kaskazini uliowajumuisha makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya na wadau wa ardhi wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga uliofanyika mjini Moshi.
Akichangia hoja hiyo mkuu wa wilaya ya Hai Bw.Lengai Ole Sabaya ameiomba serikali ibuni mfumo ambao utawabana maafisa ardhi wasipate mwanya wa kutoa hati ya kumiliki ardhi kwa zaidi ya mtu mmoja tabia ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwaa migogoro ya ardhi nchini.
Akifungua kikao hicho mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira ameitaka kamati hiyo kuangalia namna bora ya kutekeleza sera hiyo isije ikaingiliana na maeneo mengine muhimu ikiwemo sekta ya viwanda, hospital,vituo vya afya, shule, vyuo na miradi mbalimbali ya maendeleo.
