Back to top

TAWIRI YABAINISHA UMUHIMU WA SOKWE MTU (SOKWE).

13 June 2024
Share

Mtafiti wa Sokwe mtu (Sokwe)  kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Bw. Simula P. Maijo amesema Sokwe ni mnyama adhimu Tanzania ambaye kwa asili anapatikana katika mikoa ya Kigoma (Gombe na Mahale), Mkoa wa  Katavi (  Misitu ya Tongwe) na baadhi ya maeneo ya Rukwa (Kalambo). Pia, Tanzania ina Sokwe katika hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo ambao siyo wa asili katika maeneo hayo.

"Kwa Tanzania Sokwe wanakadiriwa kuwa chini ya 2500 kwa idadi. Na kati ya idadi hiyo, zaidi ya asilimia 75% wanapatika na na kuishi katika maeneo ambayo yanapatikana nje ya hifadhi za Taifa za Gombe na Mahale"  ameeleza  Mtafiti  Maijo

Mtafiti Maijo amesema kuwa, Sokwe ni wa kipekee sana na wanaumuhimu mkubwa katika mifumo Ikolojia wanayopatikana, hivyo kuna uhitaji wa dhati kuhakikisha wanyama hawa wanahifadhiwa ili kudumisha uwiano wa ikolojia wanayopatikana na kuishi ukizingatia kuwa mnyama  huyu yupo katika hatari ya kutoweka (endangered) kutokana na uharibifu wa makazi yao unaosababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, na uanzishwaji wa makazi holela ya binadamu katika maeneo yao ya asili.

Aidha, Mtafiti Maijo amebainisha  Sokwe ndiye mnyama pekee aliye na ufanano mkubwa  wa vinasaba  na binadamu ambapo kwa mujibu wa  taarifa za kisayansi zinaonesha kuwa Sokwe anashahabiana kivinasaba na binadamu kwa  zaidi ya asilimia 98%. 

Katika uhifadhi, Mtafiti  Maijo amesema  Sokwe wanasaidia sana katika kusambaza mbegu mbalimbali kutokana na vyakula wanavyokula. Kwa asilimia kubwa (kati ya 60%-80%), chakula kikuu cha Sokwe ni matunda. Katika kula matunda ya mimea ambayo ni chakula chao, Sokwe huwa wanameza pia mbegu za matunda hayo. Utafiti unaonesha mbegu iliyopita katika mfumo wa umeng’enyaji wa chakula cha Sokwe ina asilmia kubwa ya kuota ikilingwanishwa na mbegu ambazo hazikupitia mfumo huo. Hivyo Sokwe wanasaidia kuboresha mazingira kupitia usambazi wa mbegu za mimea.

 " Ingawa kuna wanyama wa spishi nyingine wanaowezesha usambazaji wa mbegu, lakini Sokwe ni wazuri zaidi katika kufanya hivyo. Hivyo ni muhimu kuhakikisha bioanuwai hii adhimu (Sokwe) inalindwa" ameeleza Maijo

Akizungumzia upande wa Uchumi Mtafiti Maijo amesema  Sokwe wanachangia pato la taifa kupitia utalii wa picha. Mfano, katika hifadhi za Taifa za Gombe na Mahale, Sokwe ndio zao kuu  la utalii. Kupitia utalii, kuna ajira nyingi za zinatengenezwa kuanzia kwa waongoza watalii, mameneja, wapishi, n.k. Pia wageni wanaokuja kuwaangalia Sokwe hulipia na hivyo kuiingizia nchi fedha za kigeni.

Vilevile Kwa upande wa tafiti, Maijo amesema
Sokwe ni mnyama muhimu katika kusoma historia ya mageuzi (evolutionary history) ya binadamu pamoja kuwezesha tafiti za dawa mbalimbali.

TAWIRI  inawakaribisha  wadau  mbalimbali  kushirikiana  na  Kituo  cha  Utafiti  wa  Wanyamapori cha Magharibi katika kuendeleza tafiti za spishi hii muhimu ya sokwe na spishi nyingine.