Back to top

TANROADS YAWEKA KAMBI BARABARA YA MOROGORO- IRINGA KUZIBA MASHIMO.

27 April 2024
Share

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema (TANROADS) Mkoani humo inaendelea na kazi ya kuziba mashimo na kukarabati barabara kuu ya Morogoro – Iringa, ikiwemo katika eneo la Kobogwa lilipo katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambapo kumetokea shimo kubwa baada ya maji kupita pembezoni mwa Kalvati. 

Mhandisi Kyamba ameeleza kuwa tayari Mkandarasi yupo eneo hilo akiendelea na kazi ambapo wanajitahidi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika.

"Mvua zimeendelea kunyesha bila kukatika na jitihada zinaendelea kufanyika kila siku, eneo hili ambalo limeleta taharuki katika barabara hii ya Mikumi, mashimo yametokea juzi, tukayaziba kidharura lakini unapoziba kidharura mvua zikinyesha tena zinaondoa ule mchanga ambao tumeuweka kwa sababu kipindi hiki cha mvua huwezi kuziba na lami, lami haikubali kipindi cha mvua mpaka jua liwake" Amesema Mhandisi Kyamba.

Mhandisi Kyamba ameongeza kuwa Kama Tanroads wanaendelea na kazi ya kuziba mashimo yote kwenye barabara hiyo kuanzia Msamvu - Mikumi hadi Iringa mpaka wayamalize kutokana na mvua kubwa, kila siku mashimo yanajitokeza kwani juzi Kalvati maji yalipita pembeni na kutengeneza shimo kubwa ndipo ikawalazimu kuleta mitambo na nyenzo za kazi, kwa sasa barabara inapitika upande mmoja na upande mwingine kazi inaendelea.

Kwa upande wake Mhandisi Aloyce Stephen kutoka Kampuni ya Kizawa ya CGI Contractor Ltd, inayofanya kazi hiyo amesema kazi imeendelea kufanyika bila kusababisha msongamano wa magari na matarajio ni kwamba magari yaemdelee kuruhusiwa kupita pande zote za barabara bila tatizo lolote.

Aidha amemshukuru Rais wa Tanzania Mhe Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapa fursa na kuwajali Wakandarasi wazawa ikiwa ni pamoja na kuwapa malipo ya kazi kwa wakati jambo ambalo linawapa nguvu ya kuwa tayari kutekeleza majukumu yao wakati wote hata kwenye kazi za dharura kama hizo.