Back to top

TANZANIA YAPOKEA DOZI 499,590 ZA PFIZER.

23 November 2021
Share

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea Dozi 499,590 za Pfizer ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali wa kuwakinga Wananchi dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Hafla fupi ya mapokezi imefanyika na kuongozwa na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam  na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Ubalozi na Taasisi zisizo Zakiserikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt.  Gwajima amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kuwakinga jumla ya Watanzania 249,795 kutokana na kupokea Chanjo dozi 499,590 za Pfizer zilizoingia kutoka Marekani kupitia mpango wa COVAX Facility.

Aidha, Dkt. Gwajima amewaagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa kwenda kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19.

"Ninawaagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi za Mikoa na Halmashauri kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa kwenda kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19. " Amesema. Gwajima.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa huduma  za Afya na Ustawi wa Jamii na Lishe OR TAMISEMI Dkt. Paul Chawote amewashukuru Wadau kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha afya ya wananchi, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuketa Maendeleo hususan katika sekta ya afya.