Back to top

Tanzania yashiriki Mkutano wa Utalii Duniani (UNWTO).

01 December 2021
Share

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii kuitembelea Tanzania pamoja na mapato yatokanayo na Utalii, suala la kutangaza utalii wa Tanzania katika nyanja za kidunia ni suala ambalo haliepukiki.

Ameyasema hayo akiwa nchini Hispania, katika Jiji la Madrid kushiriki mkutano mkuu wa 24 wa Kimataifa wa Utalii Duniani ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa  linaloshughulikia masuala ya Utalii Duniani ( UNWTO) unatarajiwa kufunguliwa leo Desemba Mosi,2021.

Ametaja moja ya kati ya maeneo ya  kutangaza Utalii huo, ni kuhudhuria mikutano mikubwa duniani ambayo Inahusisha masuala ya Utalii  ikiwemo kuja nchini Hispania ambako ndiko makao makuu ya utalii Duniani  katika jiji la Madrid, kwa ajili ya  kuhudhuria mkutano mkuu huu wa 24.

Ikiwa ni siku ya kwanza ya mkutano huo Tanzania ilipata fursa kadhaa ikiwemo kutumia  mkutano huu kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania, kuwaambia dunia nzima kwamba Tanzania ipo salama na kuwataka watalii kuja kujionea vivutio vya utalii ilivyonanvyo.

Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa, katika suala la pili katika mkutano huo, Tanzania itasaini mkataba na UNWTO wa kuweza kuwa mwenyeji wa mkutano wa 65 wa Utalii Barani Afrika ambao utafanyika kati ya tarehe 6-8 Oktoba 2022 katika jiji la Arusha.

Aidha, alisema kuwa suala la tatu kwenye mkutano huo, Tanzania imekuwa  katika  mstari wa mbele kupigania haki za Watalii ambapo watashiriki katika kufanikisha sheria ya Kimataifa inapitishwa.

Dkt. Ndumbaro alisema kuwa, mkutano huo una faida nyingi sana kwa nchi Tanzania, katika kuhakikisha kwamba tanzania inatimiza idadi ya watalii milioni tano na mapato zaidi ya bilioni sita. 

Mkutano huo wa 24 wa Kimataifa wa Utalii duniani, ni wa siku nne, kuanzia jana Novemba 30 hadi 3 Desemba, ukijumuisha ujumbe mbalimbali wakiwemo Mawaziri wa Utalii, viongozi wakuu wanchi, Mashirika ya Kimataifa ya Serikali, binafsi, wadau wa Utalii  na watu mbalimbali waalikwa.