Back to top

UCHANJAJI, UTAMBUZI MIFUGO NI BURE KWA WAFUGAJ

09 July 2025
Share

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa onyo kwa wachanjaji au watumishi watakaohusika na kazi ya kutoa chanjo na utambuzi wa mifugo kote nchini watakaojiongoza vibaya na kujaribu kuwatoza wafugaji fedha za afua ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo, kinyume na muongozo wa kitaifa uliotengezwa na Wizara kwa kuwashirikisha wadau wote na kisha ukazindiliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya Kitaifa mnamo wa tarehe 16 Juni 2025 Wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

Akizungumza katika Ranchi ya Taifa ya Kalambo (NARCO), Wilayani Nkasi na Kalambo, Mkoani Rukwa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, ameeleza kuwa, “shughuli zote za kuchanja na kutambua mifugo zinagharamiwa kikamilifu (kwa asilimia 100) na Serikali, hivyo basi wafugaji hawapaswi kulipia huduma hizo”.

“Tupo hapa NARCO Wilayani Nkasi na Kalambo, Wizara ya Mifugo tunaendelea na zoezi letu makini la utambuzi na uchanjaji wa mifugo. Tunachanja ng’ombe, mbuzi, kondoo, na kuku. Awamu hii tumefika hapa katika Ranchi ya Taifa ya Kalambo na tumekutana na idadi ya ng’ombe wapatao 36,000, wakiwemo wanaomilikiwa na Serikali kupitia NARCO, wananchi wapangaji ndani ya ranchi, pamoja na wafugaji majirani wanaozunguka uwanda huu wa malisho na machungani ya maeno ya Wilaya ya Kalambo na Nkasi ndani ya Mkoa wa Rukwa,”

“Zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa, ambapo hadi kufikia leo ng’ombe wapatao 1,500 tayari wamechanjwa na wananchi wameijitokeza kwa wingi kuonesha uelewa na mwamko wao mkubwa wa kuijenga sekta ya mifugo. Kazi hii pia inatoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo na matumizi ya teknolojia ya kidijitali kwenye utambuzi wa mifugo ili kulinda usalama wake na kusaidia Serikali kuwa na takwimu sahihi kwa mipango ya kisera, kisheria na kiuwezeshaji,” Amesema Dkt. Mhede.

Dkt. Mhede amewataka watumishi wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa zoezi hilo kuzingatia maadili na kuacha tabia ya kutoza wafugaji pesa kwani ni kinyume cha muongozo wa Serikali kwa kuwa gharama zote zimelipwa na Serikali na atakaekiuka atakuwa amekosa kukosa uadilifu wa kazi na ni usaliti kwa wafugaji na Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Robert Msalika Makungu, alieleza kuwa kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo ni hatua kubwa ya kimkakati katika kulinda afya ya mifugo na kuboresha maisha ya wafugaji, hasa katika Mkoa wa Rukwa. 

Vile vile, Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Rukwa, alieleza kuwa Mkoa umejipanga kikamilifu kutekeleza kampeni hiyo kwa ufanisi, kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo katika ngazi zote. Alisisitiza kuwa Uongozi wa Mkoa umeweka utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha hakuna mfugaji anayetozwa gharama yoyote kuhusiana na chanjo au utambuzi wa mifugo, kwani Serikali tayari imegharamia kila hatua ya utekelezaji wa zoezi hilo. Aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka muongozo huo wa kitaifa.

Bi. Mgaya Myende, mfugaji kutoka kijiji cha Nkana, Wilayani Kalambo, alisema kuwa kushiriki kwake katika zoezi hilo la chanjo kumempa faraja kubwa, hasa baada ya kupatiwa huduma ya chanjo ya mifugo yake bila malipo. Alieleza kuwa chanjo zilizotolewa ni pamoja na ya mapafu kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo, na kwa upande wa kuku zimetolewa chanjo za kideri, ndui na mafua. Alisema kuwa awali wafugaji wengi walikuwa wanaficha mifugo kwa kushindwa kumudu gharama, lakini kwa sasa anaamini wengi wataweza kuchanja mifugo yao yote.

Kwa upande wake, Bw. Benueli Makselo, mfugaji kutoka kijiji cha Sintali, Wilayani Kalambo, alifafanua kuwa amekuwa akifuatilia kwa makini agizo la Mheshimiwa Rais kuhusu kampeni hiyo. Aliona punguzo la gharama za chanjo kuwa ni neema kwa wafugaji wote akiwemo na yeye. Alieleza kuwa awali alikuwa analipa Shilingi 1,000 kwa kila ng’ombe, lakini sasa kuna ruzuku ya Serikali ambapo atachangia ununuzi wa chanjo kwa Shilingi 500, huku chanjo ya mbuzi na kondoo ikipungua kutoka Shilingi 600 hadi 300 kutokana na ruzuku ya Serikali. Pia, alieleza kufurahishwa na utoaji wa heleni za utambuzi bure, ambazo awali ziligharimu Shilingi 1,750 kwa kila ng’ombe. Alisisitiza kuwa hatua hiyo inawapa wafugaji ulinzi na urahisi wa kufuatilia mifugo yao endapo itapotea.