Back to top

VIJANA WANUFAIKA MAFUNZO YA UVUVI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MIKOPO

29 May 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amewahakikishia vijana walionufaika na mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji na ambao wameshaandaa  maandiko ya miradi kuwa watapewa kipaumbele katika kupata mikopo ili waweze kuendeleza miradi yao.

Waziri Ulega ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji katika hafla fupi iliyofanyika mkoani Mwanza Mei 29, 2023.

Amesema kuwa Wizara yake inatambua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji katika sekta ya uvuvi hivyo kupitia programu hiyo wizara imejipanga kuwasaidia wanufaika wa mafunzo hayo kupata mitaji ya kuanzisha miradi iliyobuniwa kutokana na maandiko waliyowasilisha wizarani. 

"Juhudi hizi za kutafuta mitaji ni pamoja na ruzuku na mikopo kutoka serikalini, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo. Nipende kusisitiza kuwa uanzishwaji wa vikundi, ushirika au kampuni ni fursa ya kuweza kufikiwa kirahisi na serikali sambamba na kupata fursa za mikopo yenye masharti nafuu kutoka serikalini na taasisi mbalimbali za  kifedha,"alisema

Ameongeza kuwa programu hiyo ya atamizi inaendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye nia ya kuwajengea uwezo vijana katika fani ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili waweze kujiajiri, kuongeza tija na kuongeza kipato kwa mtu na Taifa kwa ujumla. 

Aidha, amewaeleza vijana hao kuwa hatua walizoanza kuchukua za mchakato wa kuunda vikundi au kampuni kwa nia ya kuanzisha miradi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji zitasaidia  kwa kiasi kikubwa juhudi ya serikali ya kuongeza fursa za ajira kupitia sekta ya uvuvi; na kuchangia ukuaji wa sekta kutoka asilimia 2.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 8.4 ifikapo mwaka 2025/2026. 

Kwa upande wao vijana 197 walionufaika na mafunzo hayo walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo ufugaji wa samaki wakisema kuwa fursa hiyo itawawezesha kujiajiri, kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yalitolewa kwa vijana hao kwa muda wa miezi mitatu (3) katika vituo binafsi na vya kiserikali vilivyochaguliwa na wizara, ambapo vijana wamejifunza kwa vitendo ikiwemo taaluma ya ujasiriamali,  ubunifu wa shughuli mbalimbali zinazohusiana na uvuvi na ukuzaji viumbe maji ikiwemo ufugaji wa majongoo bahari, ufugaji wa samaki kwenye vizimba na mabwawa.

Mengine yalihusu utengenezaji wa chakula cha samaki, utengenezaji wa vizimba, uchimbaji wa mabwawa na utengenezaji wa nyavu. 

Programu hiyo ni endelevu na kwa mwaka ujao wa fedha wa 2023/2024, Wizara imepanga kuwawezesha vijana wengine 750 kupata Mafunzo kwa vitendo kwa vijana waliohitimu katika fani za uvuvi na ukuzaji viumbe maji nchini na wale wenye nia ya kujiajiri kupitia shughuli za uvuvi na ukuzaji.