Back to top

Wananchi wagoma kumpisha mwekezaji wa kilimo cha miwa, Kigoma.

20 April 2021
Share

Zaidi ya wakazi elfu tatu katika kijiji cha Kumtundu kata ya Mvugwe wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamegoma kuondoka kumpisha mwekezaji anayetaka kuwekeza kwa ajili ya kilimo cha miwa katika vitongoji vya Santore, Mkuyuni na Nyandurumo kijijini hapo na kuitaka serikali iwalipe fidia kabla ya kuyaachia maeneo hayo ambayo wanayatumia kwa kilimo, ufugaji na makazi.

Wananchi hao wamesema kuwa wamepewa taarifa ya kuondolewa kwenye maeneo hayo ambayo kwa zaidi ya miaka kumi na mitano wameyaendeleza na serikali imepeleka huduma za msingi ikiwa ni pamoja shule ya msingi.
.
Kwa upande wake mwenyeiti wa kitongoji cha Nyandurumo Bw.Deo Shija ameiomba serikali kusitisha zoezi hilo kwa kuwa wananchi hao wamewekeza katika shughuli mbalimbali huku Katibu Msaidizi wa Chama Cha Wafugaji Tanzania Bw.Kusundwa Wamalwa akieleza kuwa ni vyema serikali ikakutana na wananchi hao ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Aidha, Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange amesema wilaya inafanya sensa ya watu waliomo kwenye eneo la uwekezaji ili wagawiwe hekta elfu moja ambazo zimetengwa kwa ajili ya wananchi kutoka vijiji saba vya mradi ili shughuli za uwekezaji za kampuni ya Kakira toka nchini Uganda kuendelea.