Back to top

Wanasheria wa Trump wang'atuka kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

17 November 2020
Share

Mawakili wengine watatu wa timu ya kampeni ya Rais Donald Trump wa Marekani wameomba kuondosha kesi zao mahakamani zinazopinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 3 mwezi huu, hatua inayodhoofisha jitihada za timu hiyo kuyapinduwa matokeo yaliyompa ushindi mkubwa mpinzani mkuu wa Trump, Joe Biden.

Wanasheria hao Linda Kerns, John Scott na Douglas Bryan walituma ombi lao jana jioni, wakisema kuwa timu ya kampeni ya Trump imekubaliana na uamuzi wao.

Kujiondowa kwa wanasheria hao kunafuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa na kampuni kubwa kabisa ya wanasheria, Porter Wright Morris & Arthur, Alkhamis iliyopita. 

Hata hivyo, mwanasheria mwengine Marc Scaringi, amejiunga kwenye kesi hiyo na sasa atakuwa ndiye mshauri mkuu wa mashauri hayo.

Mshauri wa kisheria wa Trump, Jenna Ellis, amesema mabadiliko hayo ni ya kawaida, mwishoni mwa wiki, Trump alimtangaza mwanasheria wake binafsi, Rudy Giuliani, kuongoza timu ya kitaifa kufunguwa mashitaka ya kupinga matokeo ya uchaguzi.