Back to top

Watu zaidi ya 60 wamefariki dunia kwa ajali ya moto Morogoro

10 August 2019
Share

Watu zaidi ya 60 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 70 wamejeruhiwa katika tukio la ajali ya moto ya lori la mafuta iliyotokea leo majira ya saa moja na nusu asubuhi katika eneo la Msamvu Mkoani Morogoro baada ya betri ya lori hilo kupiga shoti na kusababisha mafuta kulipuka.

Akidhibitisha tukio hilo la ajali mbaya mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dokta Kebwe Steven Kebwe amesema juhudi za kuokoa maisha ya majeruhi wa ajali hiyo ambao hali zao ni mbaya zinaendelea kufanywa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro na miili yote ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika hospitali hiyo ya mkoa.

Akielezea chanzo cha ajali hiyo Dokta Kebwe amesema lori hilo la mafuta lililokuwa linasafirisha mafuta lilipata ajali eneo la Msamvu na muda mfupi baada ya ajali hiyo idadi kubwa ya wananchi walikwenda eneo la tukio kwa lengo la kuchota mafuta yaliyokuwa yanamwagika na mmoja kati ya watu hao akaitoa betri la gari na kusababisha kupiga shoti na kuwaka moto.

Dokta Kebwe ameongeza kuwa idadi hiyo kubwa ya watu waliofariki imechangiwa  kwa kuathiri na watu wangine waliokuwa wanashanga tukio hilo na wengi waliokufa katika ajali hiyo ni waendesha pikipiki ambao vyombo vyao navyo vimeteketea vyote kwa moto.

Maafisa wa zima moto wamejitahidi kuzima moto huo ambao umeteketeza lori lote la mafuta huku Maafisa wa  jeshi la polisi wakiongozwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Bwana Willbard Mtafungwa wakiendelea kuimarisha ulinzi ili kuepusha madhara zaidi kutokea  kwa wananchi.

Taarifa zaidi juu ya idadi ya vifo na hali za majeruhi tutaendelea kukufahamisha kadri zinapotufikia kutoka chumba chetu cha habari.

Mwenyezi mungu azilaze roho za marehemu wote mahala pema peponi amina.