Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limewafukuza kazi watumishi thelathini na mbili ambapo kati yao ishirini na tisa wakiwa ni waalimu pamoja na watendaji watatu wa kata na vijiji baada ya kuhusika na tuhuma mbalimbali ikiwemo upotevu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 50 za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Akizungumza mara baada ya maamuzi hayo, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Peter Nzalalila amesema baraza limejiridhisha kuwa miongoni mwa watumishi hao wamekuwa na vyeti vya kughushi huku watendaji wa kata na vijiji wakikwama kwa kipindi cha miaka miwili kurejesha makusanyo ya mapato ya ndani ambayo wamekuwa wakikusanya
Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wamelipongeza baraza la madiwani kuchukua hatua hiyo ambapo pia wakatumia fursa hiyo kuomba serikali kuanza kutoa huduma za awali katika hospitali ya wilaya iliyokamilika na kushindwa kuanza kutoa huduma