Back to top

WATUMISHI SEKTA YA ARDHI WATAKIWA KUTOKUWA CHANZO CHA MIGOGORO.

10 February 2024
Share

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga, amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kutokuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na badala yake wawe wasuluhishi wa migogoro hiyo.

Mhandisi.Sanga amewataka watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na weledi katika kutimiza majukumu yao bila kusahau kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu.

Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi  pamoja na kuzungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Tabora.

Vile vile, kiongozi huyo alikagua  miradi inayotekelezwa na Chuo Cha ardhi Tabora ( ARITA) pamoja na kujadili changamoto zinazokikabili chuo hicho.

Amewaasa watumishi hao wa sekta ya ardhi kuhakikisha kuwa, wanatoa majibu yenye uhakika kwa wateja na sio kuwazungusha pale wanapohitaji huduma za ardhi.

Amewataka watumishi hao kujenga tabia ya kuonyana wenyewe kwa wenyewe pindi mmoja wao anapokwenda kinyume na kanuni za utumishi wa umma. 

Akigeukia suala la kodi ya ardhi, mhandisi Sanga amesisitiza suala la ukusanyaji  mapato kupitia kodi ya pango la ardhi na kuwataka makamishna wa ardhi wasaidizi kote nchini kulisimamia jambo hilo kikamilifu kwa kuweka mikakati madhubuti.

Kwa upande wa Chuo cha Ardhi Tabora, ameutaka uongozi wa Chuo hicho kukaa na kutafakari ni namna gani watakuja na mipango ya maboresho ya kimitaala na miundombinu ya chuo ili kiweze kujiendesha katika hali ya ushindani na vyuo vingine.

Ameweka wazi kuwa, ataunda  timu ndogo itakayokuwa na jukumu la kukaa na kutafakari na hatimaye kuja na mapendekezo ya kuboresha chuo hicho.