Back to top

Wavuvi walalamika utozaji wa ushuru Bwawa la nyumba ya Mungu.

15 November 2018
Share

Wavuvi katika vijiji vinavyolizunguka bwawa la Nyumba  ya Mungu wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wamewalalamikia maafisa uvuvi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kuwakatia leseni  ya uvuvi kinyume cha taratibu na kuwatoza ushuru wa mitumbwi ambao umefutwa na serikali.
 
Wavuvi hao wamesema, leseni walizokatiwa kwa shilingi 23,000/= kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu zinaonyesha mwisho wa matumizi yake ni Disemba 31 mwaka huu badala ya miezi mitatu wakati ushuru wa mitumbwi ambao umefutwa wanatozwa shilingi 2,500/= kila mmoja kwa mwaka.

Wakizungumza na ITV kando ya bwawa hilo wavuvi hao wameiomba serikali itoe ufafanuzi juu ya masuala hayo mawili ambayo yanawakera  kwa kuwa leseni hizo zitatumika kwa miezi mitatu hadi minne na mwaka ujao watalazimika kukata leseni zingine.
 
Wakati wavuvi hao wakilalamikia hali hiyo wachuuzi wa samaki nao wamepaza sauti zao na kuiomba halmashauri ya wilaya ya mwanga ipunguze ushuru wa samaki kutoka shilingi 2,000/= hadi shilingi 1,000/= kwa kila ndoo moja ya samaki.

Hata hivyo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. Zefrin Lubuva amesema, yeye bado ni mgeni lakini anayafanyia kazi malalamiko ya wavuvi hao na kuyatolewa ufafanuzi hivi karibuni.