Back to top

WAZALISHAJI WA VYAKULA VYA MIFUGO WAPEWA ONYO, SHERIA KUWAKABILI

31 May 2024
Share

 Serikali imewataka wazalishaji na wasambazaji wa rasilimali na vyakula vya wanyama kuhakikisha bidhaa na viwanda vyao vimekaguliwa na kufikia ubora na usalama unaohitajika.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha, wakati wa kuhitimishwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).

Wataalamu hao wamefanya ukaguzi katika viwanda, wauzaji wa vyakula vya mifugo na kuwatembelea baadhi ya wafugaji wanaotumia vyakula hivyo.

Kiongoza wa timu ya ukaguzi, Dk.Zacharia Makondo, Mkurugenzi wa huduma za uchunguzi kutoka TVLA, amesema ni muhimu kwa vyakula vya mifugo kufika sokoni kama vilivyowekwa viwandani.

Amesema wanaopuuza suala la kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya nyanda za malisho na rasilimali za vyakula vya wanyama.

Makondo ameongeza kuwa katika utekelezaji wa hilo, wale wote ambao hawajasajiliwa watawafungia na hawataruhusiwa kufanya shughuli hiyo na maabara za kanda zitawezeshwa kuwa na vifaa vya kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa kwenye vyakula vya mifugo ili kuhakikisha vinakuwa salama.

Amesema baada ya kufanya shughuli hiyo kwa ufanisi katika Kanda ya Mashariki na Kaskazini, watakwenda kwenye kanda zingine kuendelea kukagua na kufanya uchambuzi wa vyakula na rasilimali za vyakula vya mifugo.

Theodata Sallema, mtaalamu wa mifugo, Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, amewakumbusha wakaguzi kufanya ukaguzi katika maeneo yao na kuhakikisha wadau wanafuata sheria.

Bi. Sallema amebainisha kuwa wale ambao wanafunga vyakula vya mifugo au madini katika vifungashio vidogo wahakikishe vinakuwa na lebo na maelezo ambayo yanaendana na mfuko wa awali ambao wameufungua kwani kwa kutofanya hivyo ni kinyume cha sheria na kuashiria udanganyifu.

Pia, amesema wizara inaendelea kuwashukuru wadau kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa na kwamba changamoto zilizobainishwa zitawasilishwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Naye Meneja wa TVLA Kanda ya Kaskazini – Kituo cha Arusha, Dkt. Rowenya Mushi amesema kanda hiyo ambayo inahudumia mikoa mitatu ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro imepata chachu ya kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula vya mifugo juu ya kupima vyakula vyao kuwa na ubora na kuleta matunda kwa wafugaji.

“Chakula bora huwa kinaleta mazao bora kwa wafugaji na hilo ndio lengo kuu la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na serikali kwa ujumla, kuhakikisha mfugaji anafuga kisasa na kupata chakula bora kwa ajili ya mifugo yao hatimaye kupata mazao bora na kupata kipato kizuri zaidi na kukuza uchumi.” Amesema Dkt. Mushi

Sambamba na hilo amewasihi wazalishaji wa vyakula vya mifugo kufikisha sampuli ya vyakula vyao katika maabara ya TVLA katika kila toleo kuhakikiwa ubora na kupatiwa elimu na ushauri juu ya vyakula hivyo ili kuleta tija kwa wafugaji wanaotegemea vyakula hivyo.

Baadhi ya wadau wa kuzalisha na kusambaza vyakula vya mifugo pamoja na wafugaji wanaotumia vyakula hivyo, wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kufanya ukaguzi na kuwafafanulia mambo kadhaa yanayohusu vyakula hivyo ili kuimarisha ubora pamoja na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Wameiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutenga muda zaidi wa kufanya ukaguzi zaidi ili kuviondoa sokoni baadhi ya viwanda ambavyo vinazalisha vyakula hivyo katika ubora wa chini na kuwauzia kwa bei ndogo wafugaji wakidhani wamepata unafuu wa bei na kuwasababishia wafugaji kutopata matokeo mazuri ya mazao ya mifugo hiyo.

TVLA inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.