Back to top

Waziri Bashungwa aliagiza BASATA kumsaidia Mzee Stima.

30 November 2021
Share

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lishirikiane na Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania,(CHAMUDATA) kumpeleka hospitali  mwanamuziki mkongwe,  Mzee Hussein Abdallah Stima mwenye umri wa miaka 85 anayesumbuliwa na maradhi ya moyo na  presha  tangu mwaka 2020 ili aweze kupata matibabu mara moja.

Mhe. Bashungwa ametoa agizo hilo leo Novemba 30, 2021 alipomtembelea Mzee Stima nyumbani kwake Buguruni kwa Mnyama jijini Dar es Salaam kumjulia hali.

“Fanyeni taratibu zote zinazohitajika haraka ili mzee wetu apatiwe matibabu, hili linawezekana". alisisitiza  Mhe. Bashungwa.

 Mzee Stima ameishukuru Serikali kwa msaada huo.

Aidha, Mzee Stima ametoa wito kwa wasanii kuimba nyimbo zinazohamasisha maendeleo ya taifa na uzalendo kwa nchi yetu.

Mzee Stima ni miongoni mwa wanamuziki nguli nchini anayejulikana  kwa umaridadi wake wa kupuliza saxophone unaowakosha watu wengi ikiwa ni pamoja na  hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.