
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali imejipanga kufanya mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo yatatumika kufanya ufugaji wa vizimba ili kutoa nafasi pia kwa shughuli za uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa na muingiliano.
Ulega ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea neo la Kampuni ya Kichina ya Tangreen iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa Samaki kwa kutumika vizimba kandokando ya ziwa Victoria, jijini Mwanza.
Amesema kuwa serikali imedhamiria kufanya hivyo ili kupunguza muingiliano wa shughuli za ufugaji wa Samaki na Uvuvi wa asili ili shughuli zote zifanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika uchumi wa buluu.
Waziri Ulega ameeleza kuwa mpango huo pia utavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika ziwa Victoria, na wao kama Serikali wanawakaribisha wawekezaji kama TanGreen kuja kuwekeza nchini.
Aidha, amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salim Mkali kuhakikisha muwekezaji huyo analindwa, na kama kutakuwa na wadokozi wenye nia ya kuirudisha nyuma kampuni hiyo wawachukulie hatua kali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Ruhumbi amesema wamejipanga kuufanya Mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa Samaki wa kufugwa katika mabwawa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amebainisha kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasisha uwekezaji wa mitaji na wamehamasisha mabenki kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na imeshaanza kutoa mikopo, huku akisema wanaendelea kuwashawishi wawekeza wakubwa wa mitaji kuwekeza katika ufugaji wa samaki na kukuza uchumi wa buluu.