Back to top

WABUNGE WAJENGEWA UELEWA KUHUSU KUPUMZISHWA KWA ZIWA TANGANYIKA

29 April 2024
Share

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendesha semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Mifugo na Kilimo, na Wabunge kutoka katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa kuhusu upumzishwaji wa Ziwa Tanganyika na utaratibu wa mikopo ya vizimba na boti za uvuvi.

Semina hiyo iliyofanyika jijini Dodoma leo Aprili 29, 2024 ni mwendelezo wa vikao, semina na warsha mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika kwa lengo la kutoa elimu na kujenga uelewa kwa Viongozi na Wananchi kuhusu Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Ziwa Tanganyika na Bonde lake.
 
Lengo la kutekeleza mkataba huo ambao unatekelezwa na nchi ya Zambia, Congo, Burundi na Tanzania ni kulinda rasilimali za uvuvi zilizopo katika ziwa hilo ambazo hivi sasa zimepungua kutokana na uvuvi usiozingatia sheria.

Akizungumza na Wabunge hao, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kuwanufaisha wananchi wake huku akiongeza kuwa wakati ziwa hilo litakapopumzishwa kwa miezi mitatu wavuvi wa maeneo hayo watapewa vizimba na maboti kwa ajili kufanya shughuli mbadala ya ufugaji wa samaki.