
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), imejipanga kuanza kutumia Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024, rasmi kuanzia mwezi Julai 01, 2024.
Hayo yalibainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando Jijini Dodoma, wakati wa kikao kazi cha kupokea maoni ya uandaaji wa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023
Kadhalika Bw. Sando aliongeza kuwa Sheria Na.10 ya Ununuzi wa Umma, ilitungwa na kupitishwa na Bunge mwezi Septemba 2023, ambapo ili iweze kutumika kwa ufanisi inategemea kanuni za ununuzi, ambazo zipo katika hatua mbalimbali na zitakamilika na kuanza kutumika rasmi katika mwaka ujao wa fedha.
"Sheria ipo tayari lakini haiwezi kutumika bila kuwa na kanuni ndio mana tuko hapa kwa ajili ya kupokea maoni ya wadau wa ununuzi kuhusu Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 ili kuiwezesha Sheria ya Ununuzi Umma ya Mwaka 2023,"alisema Sando.
Bw. Sando aliongeza kuwa anaamini Sheria hizo, zinakwenda kupunguza changamoto kwenye Rufani za manunuzi zilizokuwepo wali ambapo zilikuwa zikilalamikiwa na wazabuni.
