
Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Seliani kilichopo mkoani Arusha, kimeihimizwa kufanya tafiti za mbegu bora kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wakulima na soko, sambamba na mikakati ya kuuza mbegu zake kibiashara.
Amesema hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo wakati wa ziara ya kikazi katika TARI - Seliani, akitoa msisitizo Kituo kiwe na mbinu za kuwa na mapato ya ndani kupitia tafiti zake.
Mhe. Chongolo amebainisha kuwa huu ni wakati muafaka kwa TARI - Seliani kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya soko, huku uzalishaji huo ukichukuliwa kama fursa ya kibiashara itakayoongeza tija, mapato ya taasisi na kuongeza huduma kwa wakulima.
Aidha, amesisitiza kuwa kituo hicho kinapaswa kuendelea kufanya tafiti zinazotoa majibu ya changamoto halisi zinazowakabili wakulima na wafugaji, ikiwemo tafiti za malisho bora ya mifugo pamoja na maeneo mengine yatakayoongeza uzalishaji, tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Katika ziara hiyo, Waziri Chongolo pia ametembelea Gene Bank ya TARI - Seliani, ambayo ni hifadhi ya rasilimali za vinasaba vya mazao. Hifadhi hiyo ina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya vinasaba (germplasm accessions) 30,000, ikiwa ni hazina muhimu kwa uhifadhi wa bioanuwai ya mazao, maendeleo ya tafiti za kisayansi na uendelezaji wa mbegu bora zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi, magonjwa na wadudu.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha taasisi za utafiti ili ziwe chachu ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo kupitia ubunifu, matumizi ya teknolojia na uzalishaji wa mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
