
Timu ya Wasichana ya Tanzania inayoundwa na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu imeanza vizuri michezo yake ya kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia la Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Timu hiyo ambayo ipo jijini Moscow huko Urusi kushiriki Kombe hilo, tayari imecheza mechi 2 za kundi A na kushinda zote wakianza kwa kuifunga Kazakhstan 1-0 na kisha kuwafunga wenyeji Urusi kwa mabao 3-0.
Kwa matokeo hayo, timu ya Tanzania inayoundwa na wasichana kutoka katika kituo cha TSC cha jijini Mwanza inaongoza kundi A, lenye timu za Russia na Kazakhstan na tayari imefuzu hatua inayofuata.
Endapo wasichana hao waishio kwenye mazingira magumu wakifanikiwa kutwaa ubingwa huo, watakuwa wametetea taji lao ambalo walishinda jijini Rio de Janeiro nchini Brazil mwaka 2014.