Back to top

Lugola asema hawezi kuona majambazi yakitamba.

21 July 2018
Share

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh.Kangi Lugola amesema hawezi kuona majambazi yanaendelea kutamba ili hali jeshi la polisi lipo hivyo amemtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Simon Sirro kuwasilisha mikakati ili kuimarisha usalama ili watanzania waweze kufanya shughuli za kiuchumi saa 24.

Kauli hiyo ameitoa mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na mikakati mbalimbali aliyoiweka dhidi ya taasisi iliyoko chini ya wizara yake.

"Hatuwezi kuwa na jeshi la polisi na wakati huo huo tunakuwa na majambazi yanayotupangia ratiba, yanayotupangia muda wa kufanya kazi, majambazi yanayotuambia huku msije tutafunga mtaa"Waziri wa Mambo ya ndani,

Amesema haiwezekani Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli anakuwa anahubiri watanzania wafanye kazi halafu wako tayari kufanya kazi lakini wanapangiwa ratiba na wahalifu jambo ambalo amesema haliwezi kukubalika hata kidogo.

Mh.Lugola ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa na uhakika wa usalama wao na mali zao kwakuwa hawawezi kupewa amri ama taratibu na wahalifu.

Pia Mh.Lugola amesema mwishoni mwa mwezi huu wa Julai atakutana na wadau wa usafirishaji ili kuzungumza nao.

"Tarehe 31 ya mwezi huu nitakutana na wadau wa usafirishaji kuzungumza nao, wenye mabasi, wamiliki wa malori, madereva kwa upande wa chama chao, ili nawao wanipe mtizamo wao juu ya jambo hili, haiwezekani basi linatoka Bukoba, Kigoma, Musoma, Mwanza, linakuja linakwama Morogoro, kwanini hatuwezi kuendelea eneo hili linamajambazi." Waziri wa Mambo ya ndani