
Kocha wa Manchester United Jose Mourinho amewataka waandishi wa habari kumuheshimu baada ya timu yake kupata kipigo cha magoli 3-0 wakiwa uwanja wa nyumbani dhidi ya Tottenham.
Mourinho akionekana kukerwa na maswali ya waandishi, alinyanyuka kitini na kukatisha mahojiano na wanahabari baada ya mchezo huo uliopigwa katika uga wa Old Trafford.
Kipigo hicho cha Jumatatu usiku ndio kikubwa zaidi akiwa uwanja wa nyumbani toka aaze maisha yake ya ukocha, na pia kwa mara ya kwanza amepoteza michezo miwili kati ya mitatu ya mwanzo ya ligi.
"Nimeshinda mataji mengi ya ligi (ya England EPL) kuliko makocha wote 19 (wa timu nyengine zinazoshiriki EPL) ukiwaweka pamoja," amesema Mourinho. "Nimeshinda mataji matatu na wao mawili."
"Heshima, heshima, heshima bwana," aling'aka Mourinho akitoka kwenye chumba cha mikutano ya wanahabari.
Goli la kichwa la nahodha Harry Kane na mawili mengine yaliyofungwa na Lucas Moura yameipa ushindi wa tatu mfululizo Tottenham na kuwapandisha mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL.
Mourinho, raia wa Ureno amenyenyua taji la EPL mara tatu kwa vipindi viwili tofauti akiwa na Chelsea, wakati Pep Guardiola na Manuel Pellegrini wakishinda mara moja kila mmoja wakiwa na Manchester City.
Mreno huyo pia ameshinda mataji mawili ya ligi ya Ureno akiwa na Porto, mawili Italia akiwa na Inter Milan, na moja Uhispania akiwa na Real Madrid. Pia ameshinda mataji mawili ya klabu bingwa Bara la Ulaya. Taji kubwa zaidi alilolitwaa na Man United ni kombe la Europa mwaka 2017.
"Mnataka kama kufanya muujiza juu ya timu yangu, ambayo ilicheza vizuri na kwa mpango, tulikuwa vizuri sana lakini mmekuja hapa na mnajaribu kuugeuza mkutano huu kwa kuniangushia mzigo wa lawama," alifoka Mourinho.