Back to top

Wasiojulikana waendelea'kumtesa' Lissu,Matumaini ya kurejea Tz yafifia

29 November 2019
Share

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu amesema kwa sasa hawezi kuuhakikishia umma kwamba atarudi Tanzania licha ya hali yake kuimrika kwa kile anachoeleza  kuwa kuhofia usalama wake.

Lissu ametoa kauli hiyo nchini Kenya wakati wa mazungumzo yake na kituo cha KTN News cha nchini humo ambapo ameeleza wasiwasi wake wa kurejea Tanzania kwani bado mawazo yake anayaelekeza kwa watu wasiojulikana.

"Hali ya usalama wangu bado sio nzuri, nafikiri hakuna mtu ukiachia wale wanaoitwa watu wasiojulikana na waliowatuma, nafikiri wengine wote hawana maslahi na hawataki kuona nirudi nyumbani kesho, halafu kesho hiyo hiyo ama keshokutwa yake nipigwe risasi tena "-Mhe.Tundu Lissu.

Ameeleza kwamba bado anatamani sana kurudi Tanzania kwani dhamira yake sio kuishi uhamishoni kwa muda wa miaka miwili sasa, kwani hata yeye anatamani kurudi Tanzania kujumuika na wenzake kufanya kazi.

"Mimi sitaki na sijawahi kutaka kuishi uhamishoni, siko uhamishoni, nilienda kwa matibabu, nimeshatibiwa sasa nasubiri niambiwe, usalama wangu utakuwaje, katika mazingira halisi tunazungumzia mtu ambaye amepigwa risasi 16, amefanyiwa Operesheni 24, katika kipindi cha miaka miwili"-Tundu Lissu.

Kuhusu atakaa mpaka lini huko uhamishoni na ikiwa Tanzania ni nyumbani Tundu Lissu amesema sasa hivi yapo majadiliano ya marafiki wa ndani na nje ya nchi ya kuona ni namna gani atakaporudi Tanzania atakuwa salama, na akihakikishiwa usalama basi yeye hana neno atarudi nyumbani.

"Sasa katika mazingira ambayo bado kuna vitisho vya aina hii, watu wenye busara lazima wakae, waangalie namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu lakini nikiwa salama"-Mhe.Tundu Lissu.

Wakati huohuo Tundu Lissu ameonesha dhamira yake ya kuwania Urais wa Tanzania 2020 endapo chama chake na vyama vingine vya upinzani vyenye mrengo mmoja vitamuunga mkono na kupeperusha bendera.

"Kama chama changu na vyama rafiki vya kisiasa vya Tanzania vitanipa dhamana ya kuwawakilisha katika uchaguzi Mkuu ujao, kama mgombea Urais niko tayari kuitikia huo wito"-Mhe.Tundu Lissu.

Unaweza kufuatilia mazungumzo hapo chini.