
Washindi katika mashindano ya Olympic 2020 huko Tokyo Japan mwaka huu watalazimika kuvaa medali wenyewe shingoni mwao kutokana na tishio la virusi vya Corona katika mji wa Tokyo kwa miezi sita sasa.
Taarifa hiyo imethibitishwa na kamati ya kimataifa ya Olympic IOC leo Jumatano ikiwa ni siku 9 kabla ya kuanza kwa mashindano hayo makubwa duniani.
Rais wa IOC Thomas Bach amesema medali zitawekwa kwenye sahani na washindi wa medali hizo watakuwa wanazichukua wenyewe kisha kuzivaa shingoni.
Hizi zimekuwa ni tahadhari kali kuliko zile za EURO 2020 katika fainali kwenye uwanja wa Wembley jijini London ambapo licha wachezaji kuvishwa medali lakini pia Rais wa UEFA Alexander Ceferin alishikana mikono na golikipa wa Italy Gianluigi Donnarumma.
Na sasa hayo yamejiri huko Japan baada ya Bach kukutana na Waziri Mkuu wa Japan Yoshihide Suga kujadili namna watakavyochukua tahadhari ya Corona wakati wa mashindano hayo mjini Tokyo na kukubaliana kuwa hakutakuwa na kushikana mikono wala kuwavalisha medali washindi isipokuwa medali zitapelekwa kwao zikiwa kwenye sahani kisha watavaa wenyewe wakati wa sherehe za utoaji wa medali.