Back to top

Hawako tayari Wakulima wa korosho kukatwa asilimia 2.

29 October 2021
Share

Wenyeviti wa vyama vikuu vya ushirika vinavyosimamia wakulima wa zao la Korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi wamesema hawako tayari kuona wakulima wanakatwa asilimia mbili ya mauzo ya korosho wakati tayari serikali inakata asilimia 15 ya mauzo yote ya zao hilo, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania ikisema sheria hiyo ni mpya na imegusa mazao yote na si korosho pekee.

Wakizungumza na waandishi wa habari wenyeviti hao wameiomba serikali kuondoa makato hayo ambayo wamedai yanamzidishia mkulima wa korosho  mzigo kutona na zao hilo kuwa na makato mengi.

Hata hivyo wamesema makato hayo yamekuja ghafla pasipo kuwajulisha wakulima hivyo kunahatari ya kuleta migogoro baina ya vyama vikuu vya ushirika na wakulima huku wakiwanyooshea vidole wabunge kwa kupitisha sheria hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoa wa Mtwara, Denis Urio amesema sheria hiyo ya fedha ya mwaka 2021  kifungu No.23 iliyofanyiwa mabadiliko katika sheria ya kodi imemtaka kila mkulima, mvuvi na mfugaji kuchangia asilimia mbili ya mapato yake kwenye mapato ya nchi.

Amesema sheria hiyo imeanza kutumika tangu mwezi wa saba mwaka huu na tayari mamlaka hiyo imekuwa kitoa elimu kwa wahusiaka hivyo wakulima wakorosho hawana budi kutoa ushirikiano kwa serikali katika kukusanya kodi hiyo.