Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu ameitaka Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuanza kutoa huduma za Ushauri na Msaada wa Kisaikojia kwa njia ya mtandao ili kuweza kuwafikia watu wengi.
Dkt. Jingu ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam wakati akizindua Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kilicho chini ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii.
Dkt. Jingu amesema kuwa kuanza kutoa huduma hizo katika Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kutaongeza ufanisi na kupunguza msongamano pindi wateja wakatapo kuwa wengi Kituoni hapo.
Aidha Dkt. Jingu amesisitiza kuwa kituo hicho kina uhitaji mkubwa katika jamii kwani kuna matatizo mengi katika jamii ikiwemo mafarakano ya ndoa, kifamilia, misongo ya mawazo kutokana na ukosefu wa vipato toshelezi na ajira, kukata tamaa kutokana magonjwa sugu na ya kudumu kama kansa na mengine yasiyoambukiza hivyo kitasaidia kutoa huduma kwa wananchi ambao wamepatwa na matatizo ya Kisaikojia.
Pia Dkt. Jingu ameipongeza Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau kutoa huduma za ushauri na msaada wa kisaikolojia pindi majanga yanapojitokeza hasa majanga ya moto, mafuriko na majanga mengine akitolea mfano maafa ya moto mjini Morogoro ambapo Taasisi ilikwenda kutoa msaada kwa wahanga.
