Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda nchini kuwapokea na kuwapa ushirikiano watu wenye ulemavu ili waweze kupata fursa ya kuchangia katika shughuli za ujenzi wa Taifa kama Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inavyotaka.
Ameyasema hayo leo (Jumanne Novemba 16, 2021) baada ya kuzindua kiwanda cha kampuni ya SIKA Tanzania kinachozalisha na kusambaza kemikali zinazotumika kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali kilichopo Salasala. Pia Waziri Mkuu amefungua kinu namba mbili cha saruji katika kiwanda cha Twiga baada ya kukamilika kwa maboresho makubwa.
Akiwa kwenye viwanda hivyo kwa nyakati tofauti Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuweza kuvutia wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Pia, ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara iendelee na utaratibu wa kukutana na Wizara au Taasisi za Serikali na Binafsi nchini ili kuwahamasisha kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafanyakazi wa viwanda hivyo kuwasaidia wawekezaji hao ili wakuze zaidi biashara zao na wanufaike na uwekezaji huo.
