
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameshiriki Mkutano wa Jukwaa la Majadiliano ya Kiuchumi (Bloomberg New Economy Forum 2021 ) mkutano unaojadili masuala mbalimbali ikiwemo muelekeo mpya wa Kiuchumi baada ya athari za Uviko 19 pamoja na Mabadiliko Tabia nchi.
Makamu wa Rais ameshiriki kama mtoa mada katika mjadala unaohusu Juhudi za Pamoja za Kuijenga Upya Jamii Baada ya Uviko19 kwa Kuepuka Hatari ya Kuongezeka kwa Tabaka baina ya Masikini na Matajiri.
Akizungumza katika mjadala huo Makamu wa Rais amesema ipo haja ya mataifa yalioendelea kutoa msaada wa haraka katika mapambano dhidi ya Uviko 19 pamoja na ufufuaji uchumi kwa mataifa yanayoendelea hasa kusini mwa janga la Sahara.
Aidha amesema Tanzania hutumia sekta ya utalii katika kuchangia Pato la Taifa hivyo kufungwa kwa mipaka na kusimama kwa biashara za kimataifa wakati wa janga la Uviko 19 kumepelekea ukuaji wa uchumi kushuka.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba katika dunia ya sasa ni muhimu kuwekeza katika TEHAMA itayorahisisha na kuharakisha namna ya ufanyaji kazi pamoja na upatikanaji wa huduma hivyo, ameyaasa mashirika ya fedha ya kimataifa kuja na mpango maalum wa kuziwezesha nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kuweza kufikia mapinduzi ya TEHAMA pamoja na upatikanaji wa chanjo.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema mataifa yalioendelea ni vyema kushirikiana na mataifa ya Afrika katika tafiti za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhamishia baadhi ya viwanda ikiwemo vya Chanjo katika mataifa ya Afrika ili kutoa fursa ya waafrika kujifunza na kupata maarifa katika utengenezaji wa chanjo hizo.
