Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi limejiimarisha kwenye upande wa mafunzo mbalimbali ya medani ili kukabiliana na matishio ya uhalifu na wahalifu na kuhakikisha hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari.
.
IGP Sirro amesema hayo leo akiwa Mkomazi mkoani Tanga, wakati alipofanya ziara ya ukaguzi kwenye eneo la kambi ya mafunzo ya medani za kivita ambapo zaidi ya askari 700 wa cheo cha Mkaguzi wa Polisi wanapatiwa mafunzo ya medani kwenye eneo hilo.
.
Aidha, IGP Sirro amesema kuwa katika kuelekea kwenye miaka 60 ya Uhuru Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha amani na utulivu inazidi kuimarika nchini na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo ili kufichua uhalifu na wahalifu na wale watakaojaribu kuvuruga amani ya nchi wataendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
.
Naye Kamishna wa Operesheni na Mafunzo CP Liberatus Sabas amesema kuwa, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Kambi ya Medani za Kivita lililopo Mkomazi Mkoani Tanga ambapo askari wa Jeshi hilo watalitumia eneo hilo kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ya kijeshi.
.
Wakati huo huo IGP Simon Sirro akiwa eneo la Mombo Mkoani Tanga, amewataka wazazi na walezi kuendelea kuimarisha malezi ya familia ili kuwaepusha watoto kujiingiza kwenye vitendo vya kiuhalifu na badala yake kuwasaidi katika kuwapatia elimu na msingi wa maadili.
